MABADILIKO YA SIKU ZA IBADA SURA YA 4

SURA YA 4.

KWA JINSI GANI, KWA NINI, NA NI NANI ALIYEFANYA BADILIKO HILI
Badiliko toka Sabato ya kweli kwenda sabato ya uongo lililetwa na uasi mkuu uliotokea katika kanisa la mwanzo ambalo liligeuka na kuwa katika mfumo wa Kikatoliki wa Rumi [Roma]. Sababu zilizolisukuma kanisa hili kuitupilia mbali Sabato ya Bwana na kuichagua siku ya waabudu jua zilikuwa mbili: nazo ni hizi,

  1. Kuepuka kufananishwa na Wayahudi, ambao ushupavu wao wa dini na anguko lao viliwafanya kuchukiwa na watu wote;
  2. kutengeneza usawa ati yao na wapagani waabudu jua ili kuwaongoa wapagani waliokuwa wanaabudu jua na kuwafanya washikamane na kanisa.

Hata katika siku zile za Mitume uasi huo ulianza kujitokeza. Paulo aliandika hivi:
"Maanaile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi" (2 Wathesalonike 2:7).

Tena mtume Paulo alilitambua swala hilo vizuri sana na alionya na kutangaza yakwamba:  "Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawandamie wao"    (Mdo 20:29,30).

Ukengeufu huo kutoka katika imani ungeenea na kukua kwa kiwango kikubwa, alisema Mtume huyo.
"Ukengeufu" huo mkubwa, ama uasi, hatimaye ungemfunua "yule mtu wa kuasi [mtu wa dhambi]," "mwana wa uharibifu; yule mpingamizi [Mpinga Kristo], ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la  Mungu [Kanisa], akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu"  (2 Wathesalonike 2:3,4).

Kwa kutimiza unabii huu uliotabiriwa, imani ya Kikristo na utawala wa kanisa la Kikristo
vikabadilika kabisa katikati ya siku zile za Mitume na kule kutangazwa kwa uongofu wake
Konstantino (Constantine), Mfalme wa Rumi [Roma]. Kweli ikabadilishwa na kuwa uongo, na
upotoshaji wa imani ile ya kweli uliongezeka kasi sana kwa kiwango cha kushangaza.
"Urembo wa ibada na kawaida za ibada ambazo wala Paulo, wala Petro hakupata kuzisikia, zikaingia kanisani kimya kimya na kuanza kutumika, na baadaye zikadai kuwa zina cheo sawa na zile  zilizowekwa na Mungu.”
“Maofisa [wa kanisa] ambao Mitume wale wa zamani wasingeweza kupata mahali pa kuwaweka, pamoja na vyeo vyao ambavyo kwao [Mitume] vingekuwa havina maana yo yote kabisa, vikaanza kuleta changamoto kwa watu, na kuitwa kuwa ni vyeo vya Mitume."
WILLIAM D. KILLEN, D.D., THE ANCIENT CHURCH, Utangulizi kwa Toleo la Kwanza, uk. Xvi

Miongoni mwa maadhimisho haya ya ajabu, mapya, na ya uongo yaliyoingizwa katika
kanisa lile lililoanguka, ilikuwa ni sikukuu ya Jumapili.

Wilhelm August John Neander, mwanathiolojia mkuu na mwanahistoria wa Kijerumani toka
Heidelberg, ambaye kitabu chake cha  'HISTORY OF THE CHRISTIAN RELIGION AND
CHURCH'  kina thamani kubwa na sifa kiasi cha kumpatia cheo cha "mkuu wa wanahistoria
wa Kanisa," anatangaza kwa kusema kweli tupu:

"Upinzani kwa dini ile ya Kiyahudi ulisababisha kutangazwa kwa sikukuu maalum ya Jumapili mapema sana, naam, ikiwa badala ya Sabato.... Sikukuu ya Jumapili, kama zilivyo sikukuu nyingine zote, daima ilikuwa ni amri ya wanadamu tu, nayo ilikuwa mbali na makusudi ya wale Mitume kuweza kuanzisha amri ya Mungu kwa njia kama hii, na tangu mwanzo wa kanisa la Mitume wazo hili la kuhamisha sheria za Sabato kwenda Jumapili lilikuwa mbali nao. Labda, mwishoni mwa karne ya pili ndipo matumizi potofu kama hayo yalianza kufanyika; maana kufikia wakati ule watu wanaonekana kwamba walianza kufikiria kuwa kufanya kazi siku ya Jumapili ilikuwa ni dhambi." -----  Rose's translation from the first German edition, uk.l86.

JE KUABUDU SIKU YA SABATO KULIPIGWA MARUFUKU?
Utunzaji wa siku ya saba haukukatizwa na Wakristo wale wa kwanza kwa kipindi kirefu baada ya kupaa kwake Kristo. Mamia ya miaka yalikuwa yamepita kabla ya nguvu na uwezo wa Upapa (Papacy) kuiondoa kanisani. Kusema kweli, kamwe haijakatizwa kabisa kabisa, kwa vile siku zote kumekuwako na mbegu ya wenye haki walioendelea kuwa waaminifu na watiifu kwa Sabato takatifu ya Mungu. Hebu turejee baadhi ya maandiko yaliyoandikwa na wanathiolojia mbalimbali:-
Bwana Morer, mchungaji msomi wa Kanisa la Kiingereza (Church of England), asema
Kwamba:-
 "Wakristo wale wa zamani walikuwa na kicho kikubwa sana kwa Sabato, nao waliitumia siku hiyo kwa ibada na mahubiri. Na hapana mashaka yo yote kwamba waliipata desturi hiyo toka kwa Mitume wenyewe." DIALOGUES ON THE LORD'S DAY, uk.l89.

Profesa Edward Brerewood wa Chuo cha Gresham, London, kutoka katika Kanisa lilo hilo
asema hivi:
"Sabato ile ya zamani iliendelea kuwako na kutunzwa... na Wakristo wale wa Kanisa la Mashariki (East Church), kwa zaidi ya miaka mia tatu baada ya kifo cha Mwokozi wetu."
                                    A LEARNED TREATISE OF THE SABBATH, uk.77.
           
Mwanathiolojia mwangalifu na msema kweli na mwanahistoria, Lyman Coleman, asema
hivi:
"Kuendelea mpaka kufikia karne ile ya tano utunzaji wa Sabato ya Kiyahudi uliendelezwa na kanisa la Kikristo, lakini nguvu yake na utaratibu wake wa ibada vikaendelea kupungua pole pole mpaka hapo ilipokoma  kabisa kutunzwa."
                ANCIENT CHRISTIANITY EXEMPLIFIED, Sura ya 26, Sehemu ya 2, uk.527.

Socrates, mwanahistoria ya kanisa Myunani aliyeishi katika karne ile ya tano, ambaye kazi
yake ilikuwa ni maendelezo ya ile ya Eusebio [Eusebius] asema hivi:

"Karibu makanisa yote ulimwenguni wanaadhimisha meza takatifu ya Bwana siku ya Sabato
ya kila juma, lakini Wakristo wale walioko Alexandria na Rumi, kutokana na mapokeo fulani
ya zamani, wameacha kufanya hivyo."  ECCLESIASTICAL HISTORY v.22.2l,22, in A SELECT LIBRARY OF NICENE AND POST-NICENE FATHERS, 2d Series, Vol.II, uk.l32.

Sozomen, mwanahistoria wa kanisa mwingine wa karne ile ya tano, anathibitisha kwa
maneno haya:
"Watu walioko Constantinople, na karibu wa kila mahali, wanakusanyika pamoja siku ya Sabato, na vile vile katika siku  ya kwanza ya juma, desturi ambayo kamwe haifuatwi kule Rumi na kule Alexandria."   ECCLESIASTICAL HISTORY, vii.l9, in  A SELECT LIBRARY OF NICENE AND POST-NICENE FATHERS, 2d Series, Vol. II, uk.390.

UPOTOFU WA UKRISTO
Utunzaji wa siku ya Jumapili ulianza kipindi cha mapema katika historia ya kanisa. Walakini, kule kuingizwa kwake [Jumapili] mapema sio sababu ya kuifanya iwe halali kuadhimishwa kama wajibu ulioagizwa na Maandiko. Amri ile  tu itokayo katika Maandiko ndiyo inayotosheleza kwa jambo kama hilo. Wala hakuna amri kama hiyo inayotokana na Maandiko kwa kuiadhimisha Jumapili.

Hakuna idhini yo yote ya Maandiko kwa kuingiza mageuzi yale potofu katika kanisa lile la
kwanza, ambalo hatimaye liligeuka na kuwa Upapa. Juu ya suala hilo, Dowling, katika kitabuchake cha 'HISTORY OF ROMANISM,' anasema maneno haya:

"Hakuna cho chote kinachoushtua moyo wa mwanafunzi mwangalifu wa historia ya kale ya
kanisa kwa mshangao mkubwa sana kama kipindi kile cha mapema sana ambacho kilishuhudia uingizaji [kanisani] wa upotofu mwingi sana wa Ukristo, ambao umo katika mfumo wa Kiroma, ukiotesha mizizi yake na kukua; hata hivyo isidhaniwe kwamba waasisi wale wa kwanza wa mawazo hayo mengi pamoja na kawaida zake ambazo ni kinyume na Maandiko ya kuwa walikusudia kuvipandikiza viini hivyo vya upotofu, wakitazamia au hata kuwazia kwamba vingekua  kiasi hicho na kuzalisha mfumo mkubwa na wa kuchukiza kama huo uliojaa ushirikina na makosa mengi kama ule wa Upapa."    Thirteenth ed., i.1, Sec. 1, uk.65.

MUUNGANO WA UKRISTO POTOFU NA UPAGANI.
Hivyo ndivyo inavyoonekana ya kwamba muungano huu kati ya Ukristo potofu na upagani uliozalisha Ukatoliki wa Rumi ulikuwa ndio udongo ulimokua ule utunzaji wa sabato ya bandia, yaani, Jumapili. Mfumo huu wa Ukatoliki na Jumapili ni kitu kimoja. Vyote viwili chimbuko lake ni katika upagani, na vyote viwili vilipandikizwa katika kanisa la Kikristo kwa kipindi kile kile kimoja. 

Vyote viwili viliufagilia mbali upinzani wote, na kuwa sehemu za mamlaka zile zilizouongoza ulimwengu ule wa Kikristo. Baada ya kujizatiti, vyote viwili vikatafuta njia ya kuelezea chimbuko lao kuwa linatoka  siku zile za Mitume. Papa akadai kwamba yeye anachukua mahali pa Petro, na Jumapili nayo ikadai kwamba siku ile  ya ufufuo ndilo chimbuko lake. Madai yote mawili hayakuwa na ukweli wo wote ndani yake, wala hakuna dai lo lote katika hayo mawili lililopata kuthibitishwa [kwa Maandiko].

Hata hivyo, udanganyifu huu wa aina mbili ulikua sana sana na kupata nguvu kubwa sana, Papa akiwa ndiye Bwana wa Maaskofu na Jumapili nayo ikiwa Bwana wa siku zote; lakini kule kufanikiwa kwao [Papa na Jumapili] kulimfukuza yule Bwana wa uzima nje ya kanisa, na kumwacha humo yule Mpinga Kristo peke yake.

Mmojawapo wa watetezi (apologist) wa siku hii ya kipagani katika miaka ile ya mwanzo, Tertullian, aliyetambulikana kama mwandishi wa kanisa na Kanisa la Katoliki, aliyaandikia kitabu mataifa yale yaliyokuwa bado yanaendelea kuabudu sanamu, na katika kitabu hicho alijaribu kuiondoa hali ya kuchanganyikiwa iliyoletwa na kule kuichagua siku ile ya Jumapili kulikofanywa na Wakristo, ambayo [Jumapili] ilizusha wazo la kwamba [Wakristo] walikuwa wanageukia kabisa kwenye ibada ya jua. Yeye asema hivi:

"Kwa kujali sana uungwana wetu yatupasa kukiri kwamba wengine wanadhani jua ni mungu wa Wakristo, kwa sababu ni jambo linalojulikana kabisa kuwa tunasali tukielekea mashariki, au kwa sababu tunaifanya Jumapili kuwa sikukuu yetu.  Ni nini basi? Je, ninyi mnafanya chini ya hayo? Je, wengi miongoni mwenu, wakati mwingine kwa kujifanya kuwa mnaviabudu viumbe vile vya mbinguni (heavenly bodies), hamchezeshi vile vile midomo yenu kuelekea kule jua linakotokea? “

“Ndio ninyi ambao, kwa vyo vyote, mmeliingiza hata jua katika kalenda yenu ya juma;  nanyi mmependelea kuichagua siku yake hii [Jumapili] kuliko siku ile iliyotangulia, kuwa ndiyo siku inayofaa katika juma aidha kwa kuacha kabisa kuogelea, au kuahirisha mpaka jioni itakapofika, kwa ajili ya kupumzika na kula karamu zenu. Kwa kufuata desturi hizi, kwa makusudi mnajitenga na kawaida zenu za ibada na kuzitumia zile za wageni."     AD NATIONES, i.l3, in THE ANTE-NICENE FATHERS, Vol. III, uk.l23

Utetezi wa pekee ambao mwandishi huyo Mkristo wa zamani aliweza kutoa kwa kuichukua Jumapili kutoka kwa Wapagani ulikuwa ni ule wa kuwauliza swali hili: "Je, ninyi mnafanya chini ya hayo?" Anaonyesha kwamba ni Wapagani walio"liingiza jua katika kalenda ya juma," na hao ndio walioipendelea Jumapili kuliko ile "siku iliyotangulia,"  ambayo ilikuwa ni Sabato. Anatoa hoja yake kwa kusema kwamba kwa jinsi gani, basi, wangeweza kuwakaripia Wakristo kwa kuiga mfano wao wenyewe?  Hakika huu ni ushahidi wa kutosha kuhusu chimbuko ambako utunzaji wa Jumapili ulianzia.

AMRI YA JUMAPILI YA ZAMANI SANA IJULIKANAYO KATIKA HISTORIA.
Konstantino alikuwa Mfalme wa Rumi kuanzia mwaka 306 mpaka 337 B.K. Yeye alikuwa mwabudu jua katika kipindi cha mwanzo cha utawala wake. Baadaye alijitangaza mwenyewe kuwa ameongoka na kuwa Mkristo, lakini ndani ya moyo wake aliendelea kuwa mshabiki wa kuabudu jua.

Kuhusu dini yake, Edward Gibbon, katika kitabu chake cha 'THE DECLINE AND FALL OF THE ROMAN EMPIRE, asema hivi:
"Ushabiki wa dini wa Konstantino ulielekezwa kwa bidii zaidi kwenye jua, Apolo (Apollo) wa miungu ya Wayunani na Warumi; naye [Konstantino] alipendezwa kuwakilishwa kwa ishara  za mungu huyo wa nuru na mashairi.”

Yeye ndiye aliyeiweka Amri ya Jumapili ya zamani sana ijulikanayo katika historia ni ile ya Konstantino iliyotangazwa mwaka 321 B.K. Inasomeka hivi:

"Katika siku tukufu ya jua hebu mahakimu na watu wale wanaokaa mijini wapumzike, na viwanda vyote vifungwe.”  Mfalme huyu alizungumzia pia kuhusu watu wa vijijini alisema hivi:-

“Walakini huko vijijini [mashambani] watu wale wanaoshughulika na kilimo wanaweza kuendelea na kazi zao kwa uhuru na kwa kulindwa na sheria hii; kwa sababu mara nyingi hutokea kwamba siku nyingine yo yote haifai sana kwa kupanda mbegu za nafaka au kwa kupanda mizabibu; isije ikawa kwa kupuuzia wakati ule unaofaa kwa shughuli kama hizo mibaraka ile ya mbinguni ikapotezwa. “    CODEX JUSTINIANUS, lib.3, tit.l2,3; translated in PHILIP SCHAFF, D.D.,HISTORY OF THE CHRISTIAN CHURCH (Seven-volume edition, l902), Vol.III, uk.380.)


Rejea
WILLIAM D. KILLEN, D.D., THE ANCIENT CHURCH
Rose's translation from the first German edition,uk.l86.
Wilhelm August John Neander, 'HISTORY OF THE CHRISTIAN RELIGION AND CHURCH'

Ahsante, Mungu akubariki

No comments:

Post a Comment