SURA
YA 1
BADILIKO
KATIKA UTUNZAJI WA SIKU YA SABA
Mahali fulani katika
zama za giza katikati ya siku zile za Kristo na siku zetu, utunzaji wa Sabato
umebadilishwa kutoka siku ya saba ya juma kwenda siku ya kwanza.
Ni hakika ya kwamba
amri ya Mungu inahusu kuitakasa na kuitunza siku ya saba kama Sabato. Hakuna
uwezekano wowote wa kukosa kuelewa maana yake hapa. Amri ni hii:
"Ikumbuke siku
ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku
ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe,
wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama
wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita
BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku
ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa." (Kutoka
20:8-11).
Pia ni hakika kwamba
hakuna amri nyingine yo yote iliyotolewa katika Maandiko Matakatifu inayoitaja
siku nyingine au siku iliyo tofauti na hii. Biblia, katika utimilifu wake wote,
yaani, Agano la Kale na Agano Jipya, inaamuru, inathibitisha, inatetea, na
kufundisha utunzaji wa siku ya saba kama Sabato. Vivyo hivyo ni kama ilivyo hakika kwamba
makanisa mbalimbali yenye waumini Wakristo leo hii katika kila sehemu ya
ulimwengu huu, ukiacha tofauti chache mno zilizo za muhimu, wanaitunza siku ya
kwanza ya juma kwa pamoja, nao wanajiunga pamoja katika kuutetea utunzaji wake.
Basi, inaonekana ya
kwamba kuna dosari kati ya uzoefu wa siku hizi wa makanisa mengi katika suala
hili la utunzaji wa Sabato na yale
mafundisho yaliyo wazi kabisa ya Biblia.
Dosari hii
inayoonekana wazi imeyasumbua mawazo ya wengi, na kufanya iwepo haja halisi ya
kupata maelezo sahihi na yanayoaminika juu ya historia ya nyuma inayohusu
badiliko hili katika utunzaji wa Sabato, wakati gani badiliko hili lilitokea,
na sababu za kufanya badiliko hili. Kwa hiyo itatupasa kutafakari kwa makini
maelezo ya Biblia yahusuyo kuanzishwa kwa Sabato miongoni mwa wanadamu, na
sababu zitokanazo na fikara zake Mungu kwa kuamuru itunzwe katika mojawapo ya
amri zake kumi.
SHERIA ILINENWA NA KUANDIKWA NA YEHOVA
Sheria pekee ya
Mungu inayojulikana miongoni mwa wanadamu iliyoagiza utunzaji wa Sabato
inapatikana katika Biblia, nayo imekwisha kudondolewa katika ukurasa huu.
Ingetupasa kuonyesha wazi ya kwamba amri hii ilinenwa, pamoja na amri zile
nyingine tisa, kwa kinywa chake Yehova Mwenyewe.
"BWANA
[YEHOVA] akasema nanyi kutoka kati ya
moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.
Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri
kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za
mawe." (Kumb 4:12,13).
Amri hizi kumi,
ikiwamo amri hii ya Sabato, ziliandikwa kwa kidole cha Mungu Mwenyewe juu ya
jiwe la kudumu. "Akaziandika juu ya mbao mbili za mawe." (Kumb 4:13).
"Mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda
[kidole] cha Mungu." (Kutoka 31:18).
Sheria hii inasemwa
katika Maandiko kuwa ni "ya haki," "ya kweli,"
"nzuri," na "kamilifu." "Tena ulishuka juu ya mlima
Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli,
na amri nzuri na maagizo." (Nehemia 9:l3).
"Sheria ya
BWANA ni kamilifu" (Zaburi l9:7).Sheria hii inao wajibu wote umpasao
mwanadamu.
KRISTO HAKUBADILI SHERIA
Halikuwa kusudi lake
Kristo kubadili, kuondoa, kutangua, wala kuibatilisha sehemu yo yote ya sheria
hii. "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja
kutangua, bali kutimiliza." (Mathayo
5:l7).
Badala ya kuitolea
sheria hiyo sifa mbaya, Kristo alikuja kuifanya iadhimishwe. "BWANA akapendezwa kwa ajili ya haki
yake, kuitukuza sheria na kuiadhimisha." (Isaya 42:21). Naam, kwa kadiri
Sabato inavyohusika, Kristo aliitunza, pamoja na kila amri nyingineyo.
"Siku ya sabato
akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake." (Luka4:16). Kusema
kweli, imani kwa Kristo, badala ya kuiweka sheria kando, inaithibitisha na
kuiimarisha. "Basi, je! twaibatilisha
sheria kwa imani hiyo? Hasha! kinyume
cha hayo twaithibitisha sheria." (Rum 3:31).
Sheria hii ya Mungu,
ambayo ndani yake imo amri ya Sabato, inatangazwa na Paulo kuwa ni "ya
rohoni," "takatifu," "ya haki," na "njema." "12Kwa maana
twajua ya kuwa torati [sheria] asili yake ni ya rohoni." 14Basi torati
[sheria] ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema." (Rum
7:12,14).
Sheria hii ni lazima
ishikwe kama sharti la kupata uzima wa milele. "Heri wale wazishikao amri
zake, wawe na haki kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango
yake." (Ufu 22:l4, Tafsiriya King James Version).
Naam, hiyo ndiyo
kanuni, au kipimo, ambayo kwayo
ulimwengu wote utahukumiwa. "Semeni ninyi, na kutenda kama watu
watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru." (Yakobo 2:12).
.
SHERIA BADO INA NGUVU
Kwa hiyo,
linaonekana kuwa ni jambo la ajabu kwamba utunzaji kama huo wa Sabato ungekuwa
umebadilishwa hata kidogo. Sheria hii ya
Mungu bado ina nguvu. Sheria hii
inaamrisha utunzaji wa siku ya saba ya juma.
Lakini siku hiyo haitunzwi hivi
sasa na watu wengi mno wanaokiri ya kwamba wao ni watu wa Mungu.
Hata hivyo, sheria
hii haibadiliki, bado ina nguvu, na hiyo ndiyo kipimo cha hukumu yake Mungu.
Siku nyingine imewekwa badala ya siku iliyoamriwa. Siku hiyo ilitoka wapi? Kwa nini imewekwa badala ya
ile iliyokuwapo? Je, utunzaji wa siku hii [nyingine]
unakubalika na Mungu? Haya ndiyo maswali ambayo sasa sisitutayashughulikia.
Ahsante na Mungu
akibariki
No comments:
Post a Comment