KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UJANA SEHEMU YA 3

Katika waraka huu nimeona ni vema tukakumbushana kuhusu ufahamu wa nyakati tunazoishi. Hii ni kwa sababu nyakati(muda) zina mchango mkubwa sana juu ya kile ambacho kinatokea katika maisha ya mwanadamu.
Januari 30, 2011 nikiwa nimelala nilisikia sauti ya mtu ikisema ‘majira, majira, majira’. Katika kutafakari ujumbe huu ilinisumbua sana kujua majira yamefanya nini?   Baada ya kutafakari kwa muda kuhusu jambo hiili ndipo likaja wazo kuhusu, ufahamu juu ya majira/nyakati tulizonazo.
Katika kile kitabu 1Mambo ya Nyakati 12:32 maandiko yanasema “Na wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao vilikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao” Ukisoma mstari huu kwenye tafsiri ya kiingereza toleo la BBE, Biblia inasemaAnd of the children of Issachar, there were two hundred chiefs, men who had expert knowledge of the times and what it was best for Israel to do, and all their brothers were under their orders’.
Naamini umeliona jambo hili, ufahamu waliokuwa nao wana wa Isakari uliwafanya ndugu zao wote (taifa) kuwa chini ya amri (uongozi) yao. Hii ni kwa sababu kutokana na ufahamu wa nyakati waliokuwa nao wana wa Isakari waliweza kuwaongoza ndugu zao kwa kuwaelekeza nini wanapaswa kufanya kijamii, kiroho, kiuchumi, kiusalama nk katika nyakati walizokuwa wakizipitia. Naam kadri taifa la Israeli walivyokuwa wakitekeleza maagizo wanayopewa na wana wa Isakari ndivyo walivyofanikiwa pande zote.
Ufahamu huu ndio uliowasaidia kujua yawapasayo Israeli kuyatenda kwa kila majira. Ufahamu wa muda waliokuwa nao wana wa Isakari, uliwapa Israeli, kujua majira yaliyopo juu yao yanaashiria nini na nyakati zilizoko juu yao zimebeba makusudi gani ndani yake?
Naam hata sasa Mungu anataka watoto wake wawe na ufahamu wa nyakati, ili wajue yawapasayo kufanya kwa kila nyakati ambazo wanazipitia katika maisha yao. Kwa mujibu wa andiko hili katika Taifa la Israeli Mungu aliinua watu mia mbili tu, ambao ndani yao walipewa neema ya kujua nyakati na zaidi kile ambacho watu wa Taifa lao wanapswa kukitenda ndani ya nyakati husika. Hii ina maana hata sasa kuna watu ambao sababu kubwa ya wao kuletwa duniani ni kuwa na jukumu kama lile la wana wa Isakari katika familia, koo, kabila, makanisa na taifa pia.
Kwa hiyo ni jukumu lako kufuatilia jambo hili kwa undani ili kama wewe ni mmoja wao basi ukae mkao wa kuhakikisha unazjiua vyema nyakati ambazo, wewe binafsi, familia, kabila, jamaa, kanisa, Taifa  nk mnapitia, na zaidi kujua nyakati ambazo zinakujua mbele yako/yenu ili uweze  kushauri ipasavyo kwenye kila nyanya.
Katika kitabu cha Muhubiri, Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu” (Muhubiri 3:1). Kwa hiyo Mungu anaposema kuhusu majira ina maana kuna wajibu/mambo ambayo mtu anapaswa  kuyafanya ndani ya majira husika. Naam Mungu anataka watoto wake wajifunze kufikiri kwa kuzingatia muda au nyakati alizowawekea.
Ni muhimu sana watu wa Mungu wakajifunza kufikiri ki-muda, naam muda/nyakati ziongoze kufikiri kwao. Biblia inasema ‘Basi anagalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu nini yaliyo mapenzi ya Bwana’ (Waefeso 5:15-17).
Ukisoma nyaraka za Mtume Paulo utagundua kwa kiwango kikubwa alijua sana umuhimu wa ‘wandugu’ kuwa na ufahamu kuhusu nyakati ili waweze kufikiri kwa kuongozwa na muda au nyakati. Paulo alilitaka kanisa la Efeso lijue kwamba liko katika nyakati za ‘uovu’, muda wao umetekwa na kuvamiwa na roho ya ‘uovu’. Hivyo ili kuzirejesha nyakati kwenye kusudi la ki – Mungu wandugu walipaswa kuenenda kwa hekima wakitafuta kujua kila siku nini ni mapenzi ya Mungu juu yao, ndoa zao, kazi zao, nchi yao nk.
Naam ndani ya nyakati/muda kuna siri nyingi sana, katika mfululizo huu nitakuonyesha ni kwa namna gani mwanadamu anapaswa kufikiri ki muda, matokeo yake ni nini na mwisho afanye nini kushirikiana na nyakati ambazo Mungu anazileta kwenye maisha yake.

No comments:

Post a Comment