JINSI YA KUKUA KIROHO



Jinsi ya kukua KIROHO:
Hakikisha kila siku unapata muda wa kuzungumza na Mungu.


Je! Utawezaje kuzungumza na Mungu? Fuata haya maelekezo yafuatayo;


- Tenga muda maalumu wa kusoma neno la Mungu pamoja na maombi. Hapa unatakiwa utafute sehemu ambayo ni kimya na isiyo na watu. Pia unapaswa uwe wewe pekeyako kwa maana huu ni wakati wako binafsi wa kuongea na Mungu.


- Andaa vifafa utakavyo vitumia katika kuongea kwako na Mungu. Chukua note book (daftari), kalamu, Biblia yako, na ikibidi radio ndogo au muziki kwa ajili ya kusikiliza nyimbo za taratibu za kuabudu.


Muda huu ni wako wewe na Mungu; sahau yote uliyoyaacha huko nyumbani, kazini, n.k. Tumia fursa hii kusoma neno la Mungu, kumwabudu Mungu, pamoja na kuomba.


Najua kila kitu chaweza kuwa kigumu mwanzoni, lakini unaweza ukaanza kwa kutumia dakika kumi kila siku ukiwa PEKE YAKO alafu utaona jinsi Mungu anavyozidi kukuwezesha siku baada ya siku.

Hakikisha unaheshimu ratiba yako siku zote. Endapo ukiona muda wa mchana unakubana; basi tafuta nafasi usiku ambayo itakupa faragha na Mungu. Jambo hili unaweza ukalifanya nyumbani, kazini, hata mahali po pote pale unapoona unapata nafasi ya kuwa peke yako na Mungu katika sehemu yenye utulivu.


Siku zote neno la Mungu linaweza kukupa jambo jipya usilolifahamu. Je! Wapenda kuyafurahia matunda ya kuongea binafsi na Mungu? Jibu lake ni hili:


TENDEA KAZI KILA KITU AMBACHO MUNGU AMESEMA NAWE. Katika hatua hii hapa panahitajika kitu kinachoitwa UTII. Maana ya UTII ni kutekeleza kila kitu hata kama wewe binafsi unaona nafsi yako haitaki. Kutii maana yake ni kutekeleza. Basi endapo neno la Mungu likikutaka kutubu au kubadili mwenendo wako; wewe tii kila kitu ambacho Mungu amesema nawe. Ukizingatia hayo utaona kila siku imani yako na ufahamu wako juu ya neno la Mungu unaongezeka.


ZINGATIA KWAMBA: Ukristo pasipo maombi ni BURE. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:


"Lakini Yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba." (Luka 5:16)


Yesu alikuwa na desturi ya kujitenga na watu ili apate faragha ya kuomba. Tukisoma Biblia ya Kiingereza inasema: "So He Himself often withdrew into the wilderness and prayed." (Luke 5:16) Neno "...OFTEN..." linamaanisha kuwa tendo hilo Yesu alikuwa analifanya kila mara (yaani ilikuwa kawaida yake kufanya hiyo - kujitenga na watu kwa ajili ya kupata ufaragha wa maombi). Je! Wewe wadhani Ukristo wako pasipo maombi utaweza kumshinda Shetani?



  Badilika sasa; jitahidi kila siku upate muda wako binafsi ukiwa pekeyako faragha kwa kuongea na Mungu. Japokuwa unaweza ukawa na desturi ya kulijadili neno la Mungu ukiwa na watu mbali mbali; lakini fahamu kuwa unapaswa pia kuwa na muda wako binafsi wa kuongea na Mungu kila siku ukiwa wewe peke yako na Mungu tu. Ukizingatia hayo utaona mabadiliko makubwa sana katika imani yako. Fanya sasa nawe utabarikiwa.

No comments:

Post a Comment