KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UJANA SEHEMU YA 2



1

Katika sehemu ya kwanza tuliangalia changamoto kubwa tano ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana na hivyo kuathiri uhusiano wao na Mungu.

Biblia katika Mithali 1:4 inasema ‘Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari. Pengine huu ni msatri wa ujumla wenye lengo la kumsaidia kijana awe mwenye tahadhari, mwangalifu, na ajifunze kufikiri kibiblia na kuchukua tahadhari kubwa kabla kabla ya kutenda, naam huku akitumia vema maarifa apatayo kuzishinda changamoto zenye kumkabili kila siku. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitakazomsaidia kijana kuzikabili changamoto mbalimbali;
  • Kijana atafute kujua nini kusudi la Mungu kumleta duniani

Wafilipi 2:13 inasema ‘Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema’. Tambua kwamba kabla hujazaliwa alikujua na akakuwekea kusudi lake unalopaswa kuliishi, maana umeumbwa ili uyatende mapenzi (kusudi) ya Mungu hapa duniani. Naam ufahamu wa kusudi la Mungu kwako utakusaidi kuishi kwa malengo na hivyo kukuepusha na kuifuatisha namna ya dunia hii.
2Katika Warumi 12:2 imeandikwa ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu’. Kijana mwenye kujua wajibu wake duniani katika kulitumikia kusudi la Mungu atajizuia na kujiepusha na makundi mabaya, kuipenda dunia, atatumia vizuri fursa ya teknolojia kwa utukufu wa Mungu na kuwa na matumizi mazuri ya muda.
Kijana huyu atatumia muda na nguvu zake ipasavyo katika kufanya kazi zenye kumsaidia kujikimu kimaisha ikiwa ameajiriwa au amejiajiri, na ambaye anasoma atazingatia masomo kwa sababu anajua anakokwenda, hivyo hataruhusu mambo ya kipuuzi yaharibu ndoto yake (Waefeso 5:15-17 na Mhubiri 12:1). Hivyo ni jukumu lako kumuuliza Mungu ili upate kujua kwa nini upo duniani. Hata hivyo, wokovu, ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu, kuomba kimaswali na vipawa ulivyopewa ni funguo muhimu za kukusaidia kuelewa kusudi la Mungu kwako.
  • Kijana ajifunze kuishi kwa imani

Waebrania 10:38 inasema ‘Lakini mwenye haki ataishi kwa imani; Naye akisi-sita, roho yangu haina furaha naye’. Pia katika 1 Yohana 2:14 imeandikwa ‘Nimewaandikia, ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi, mmemshinda yule mwovu’. Ili aweze kuishi kwa imani ni lazima kijana adumu kuongeza ufahamu wa neno la Mungu na kulitenda. Kwa kuwa chanzo cha imani ni kusikia na kusika huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).
Neno la Mungu likikaa kwa wingi litaumba imani kubwa ndani yake ambayo itamsaidia kushinda kila changamoto zinazolenga kumuondoa kwenye imani husika. Maarifa yatokanayo na neno la Kristo yatamjengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuzikabili changamoto za ujana. Naam kuishi kwa imani kutamsiaida kijana kudumu kuwa mwaminifu na kudumu kumpenda Mungu bila kuifuatisha namna ya dunia hii na tamaa zake (Mitahli 12:1a, 1 Timotheo 4:13 – 16, Ayubu 22:19 na Waefeso 5:6).
  • Kijana ajifunze kuenenda kwa roho
3
Kuenenda kwa roho ni wito wa Mungu kwa vijana leo ili waweze kuzishinda changamoto za ujanani. Biblia katika wagalatia 5:16 inasema ‘Basi nasema enendeni kwa roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili’. Kuenenda kwa roho ni kumpa nafasi Roho Mtakatifu ya kuongoza maisha yako sawasawa na mapenzi ya Mungu kwako.
Katika kuenenda kwa roho, siku zote, kijana anapaswa kutafakari mambo yoyote yaliyo ya kweli, ya haki, safi, yenye kupendeza, yenye sifa njema na yenye kupendeza      (Rejea Wafilipi 4:8 na Warumi 8:5). Ukweli ni kwamba kijana hawezi kuzikwepa kabisa changamoto za mwili kwa sababu mwili ni sehemu ya maisha na siku zote mwili hutamani ukipingana na roho (Yohana 3:6 na Wagalatia 5:16).
  • Kijana ajifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatime kuhusu mwenzi wa maisha.


Najua vijana wengi sana wamejiwekea vigezo vya wenza ambao wangependa waje kuishi nao kama wanandoa. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya vigezo vyao ni vya kimwili na ni kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao. Fahamu kwamba licha ya wewe kuwa na vigezo vya mtu unayefikiri anafaa kuwa mwenza wako na Mungu naye naye ana vigezo vya mtu anayejua anayekufaa. Naam suala la nani atakuwa mwenza wako kwa Mungu ni kipaumbele muhimu sana na ndiyo maana unapaswa kumshirikisha kwa asilimia zote ili akuongoze kufanya maamuzi sahihi (Mithali 19:14, Isaya 55:8, Mithali 16:1 na Yeremia 29:11).
4Ni muhimu kijana awe makini kuhusu maamuzi anayofanya katika kitafuta mwenzi wa maisha ili yasije kuharibu kusudi la Mungu juu yake. Kijana anapaswa kujiepusha na makosa mbalimbali katika kutafuta mwenza ikiwa ni pamoja na; Kutokumshirikisha Mungu katika kutafuta mwenzi wa maisha, kufanya maamuzi ya mwenzi wake atakuwa nani ndipo aanze kuomba, Kuficha dhambi, kuwa na vigezo binafsi visivyo sahihi, na kufanya maamuzi kabla ya wakati.
Naam kuhusu vijana walioko kwenye ndoa, ni muhimu vijana hao wakajua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu na kwamba hakuna isiyo na mapungufu, hivyo katika ndoa suala muhimu ni kila mmoja kusimama vema kwenye nafasi yake na kuchukuliana katika mapungufu yenu huku mkilenga kutafuta na kutenda makusudi ya Mungu ya kuwaunganisha.
Changamoto ni sehemu ya maisha kwa vijana, na madam tupo katika dunia hii, hakuna namna kijana atishi bila kuzikabili changamoto husika, naam jambo muhimu kijana ni kuwa makini na maisha yake akijua nafasi yake katika ufalme wa Mungu ili adumu kuyatenda mapenzi ya Mungu katika siku zake. Ni imani yangu kwamba somo hili limekuongezea maarifa katika kuzikabili na kuzishinda changamoto mbalimbali za ujanani.
Mungu wangu na akubariki na kukusaidia maana ndiye aliyeniambia ‘…utaiinua misingi ya vizazi vingi…’ (Isaya 58:12)
Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.

No comments:

Post a Comment