Ibada za maawio ya jua zimetajwa katika
Biblia. Lakini kile ambacho Mungu anasema kuhusu desturi hii si kile
unachotarajia. Angalia mafungu haya ya kushangaza. Nabii Ezekieli alikuwa
akionyeshwa, katika njozi, unabii wa muhimu juu ya dhambi za watu wa Mungu
katika wakati wetu.
Muktadha mzima wa mafungu haya unahitaji
kuchunguzwa kwa uangalifu ili kuelewa laana kuu ambayo Mungu anaijenga kuelekea
kwenye hitimisho Lake:
Hebu turejee kitabu cha Ezekiel, tuone unabii
kuhusu mambo haya tunayoyaangalia;
“…Utaona tena machukizo makubwa mengine
wanayoyatenda…na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi…Akanileta mpaka ua
wa ndani wa nyumba ya Bwana, na tazama, mlangoni pa hekalu la Bwana, kati ya
ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo
hekalu la Bwana, na nyuso zao
zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. Basi,
akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo…wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa
maana…wamerejea nyuma ili kunikasirisha…Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa
ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia
masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.” (Ezek. 8:13-18)
Kushika ibada za maawio ya jua ni
jambo kubwa kwa Mungu!
Anachukia sana kitendo hiki kiovu kiasi kwamba hatimaye atawaangamiza kabisa
wale wote wanaodumu kuzifanya (Ezek. 9)!
Si “jambo dogo” kwa Mungu kwamba mamilioni
wengi wanayafanya haya kila Isita! Inaweza kuonekana “maridadi,” “jambo
la kidini”, na “linalogusa sana” kwa wale wanaolishiriki, lakini Mungu
amewakataza watu wake wa kweli kubuni kawaida na fikira zao za kidini.
Hapendezwi katika kile ambacho watu wanaweza kujisikia au kufikiri
ni sahihi wao binafsi. Anapendezwa na wale ambao wanajali kile anachokifikiria!
Kulingana na Mungu, ibada ya jua ya kale, iliyovishwa vazi zuri na kofia za
Isita, ni namna ya ufungashaji wa kisasa wa desturi ya zamani sana, ambayo ni
ibada ya sanamu ya kipagani.
Fikiria maneno ya Mungu mwenyewe katika
Kumbukumbu la Torati 12:28-32:
“Maneno haya
nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza...Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia
mbali… nawe…kuketi katika nchi yao; ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata… wala
usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, ‘Mataifa haya waitumikiaje miungu
yao? Nami nifanye vivyo.’ Usimtende
kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana,
ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao...Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala
usilipunguze.”
Mungu huwaambia Wakristo wasichanganye kilicho
cha uungu na kilicho cha kipagani—au ukweli na uongo! Usikubali watu wakuambie
kwamba kile asemacho Mungu hakifanyi tofauti. Kinafanya!
Maandazi ya Moto Yenye Alama ya
Msalaba
Nilipokuwa katika darasa la kwanza, watoto
wote katika darasa langu walipaswa kila mmoja kuimba wimbo wa peke yake
aliouchagua. Sitaweza kusahau wakati huu wa kutisha. Nilijisikia aibu sana
kiasi kwamba nilichagua ule wimbo mfupi kabisa kutoka kwenye kitabu chetu
kidogo cha nyimbo, “Maandazi ya Moto Yenye Alama ya Msalaba,” na kuuimba mbele
ya darasa. Kwa kweli sikuwa na wazo la nini nilichokuwa ninaimba. Japokuwa
ulikuwa mfupi (ulikuwa na maneno kumi-na-tano tu), sijaweza kusahau funzo la
maana yake.
Angalia Yeremia 7:18: “Watoto huokota kuni, na
baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia
wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate
kunikasirisha mimi.” Mikate iliyokuwa inatolewa kwa malkia wa mbinguni ilikuwa
ni haya haya maandazi ya moto yenye alama ya msalaba ambayo mamilioni ya watoto
leo huimba juu yake (Alexander Hislop, Babeli Mbili, uk. 107). Kile
kinachoonekana kutokuwa na hatia si safi hata kidogo.
“Malkia wa mbinguni” ni nani?
Ashtorethi—Malkia wa Mbinguni
Ibada ya Asitate (Isita) daima iliambatana na
ibada ya Baali au kuabudu jua. Asitate alikuwa mke wa Baali. Angalia kwamba
jina lingine la Asitate lilikuwa ni Ashtorethi. Nukuu ifuatayo inaliweka hili
wazi. “Neno Isita lenyewe lina maana gani? Si jina la Kikristo. Linabeba asili
yake ya Kikaldayo kwenye paji lake la uso. Isita halina maana nyingine
zaidi ya Asitate, moja ya cheo cha Beltisi, malkia wa mbinguni…Sasa,
mungu mke wa Waashuru, au Asitate, anatambulishwa kuwa ni Semiramisi na Athenagorasi
(Legatio, kit. ii. uk. 179), na Lucian (De Dea Syria, kit. iii.
uk. 382)…Sasa, hakuna jina ambalo lingeweza kuonyesha tabia halisi ya
Semiramisi, kama malkia wa Babeli, zaidi ya jina la ‘Asht-tart,’ kwani hilo
maana yake ni “Mwanamke aliyejenga minara”…Basi, Ashturit…ni wazi kwamba ndilo
hilo hilo la Kiebrania ‘Ashtorethi’” (Alexander Hislop, Babeli Mbili,
ku. 103, 307-308).
Angalia nukuu hii hitimishi kutoka Ensaiklopidia
ya Microsoft Encarta Multimedia: “Ishita alikuwa Mama Mkuu, mungu mke wa
uzazi na MALKIA WA MBINGUNI.” Hivyo, kiuhakika, Ashtorethi (Ishita) alikuwa
mjane kahaba mama/mke wa Nimrodi, Semiramisi, kama wengi wa wanahistoria wa
kale wanavyoshuhudia! Sasa Isita imewekwa imara kwamba si kitu kingine zaidi ya
Ashtorethi wa Biblia! Sasa tunaweza kuchunguza maandiko yanayoonyesha jinsi
Mungu anavyoitazama ibada ya huyu mungu mke wa kipagani—kwa jina lolote!
Mungu Huiita Isita Uovu
Sasa kwa kuwa tunajua kuwa Isita ni mungu mke
Ashtorethi, tunahitaji kutazama kwenye Biblia na kuona kile Mungu
anachofikiria. Angalia fungu hili: “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu
mbele za macho ya Bwana...Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi
[Isita]” (Amz. 2:11, 13).
Muktadha unaonyesha kwamba Mungu aliruhusu
watu Wake wachukuliwe kutoka kwenye
nchi yao kwenda matekani kama matokeo ya dhambi
hii! Huendelea, ikielezea jinsi ambavyo Mungu aliwakomboa watu Wake mara
kwa mara tena kwa njia ya waamuzi. Baada ya kila ukombozi, Israeli aliwarudia
miungu hao hao wa uongo, kitendo ambacho kilileta utekwaji nyara mara nyingine,
kwa kushindwa na mataifa yaliyokuwa yakiwazunguka. Kamwe hawakuonekana
kujifunza kama fungu la 19 linavyoweka wazi. “Lakini ikawa, wakati alipokufa
mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu… kwa kuifuata miungu mingine…na…hawakuacha
matendo yao, wala njia zao za ukaidi.” Katika sura ya 10 fungu la
6, Israeli anarudia mtindo huu wa ukaidi. Na Mungu, vivyo hivyo, bado hukiita
kitendo hiki uovu.
Ibada za Baali na Ashtorethi zilijitokeza
wakati wa Samweli. Samweli aliwaambia Israeli, “…iondoleeni mbali miungu
migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana
mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake...Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa
Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake” (1 Sam. 7:3-4).
Baadaye, katika 1 Samweli 12:10-11, Samweli aliielezea historia ya Israeli
hadharani. Aliwakumbusha kwamba waliendelea kurejea katika kumtii Mungu, kisha
kurudia ibada ya sanamu tena na tena!
Imesemwa kwamba “Kitu pekee ambacho mwanadamu
amejifunza kutokana na historia ni kwamba hakuna mtu anayejifunza kutokana na
historia.” George Santayana alienda mbele zaidi na kusema, “Wale wasiojifunza
funzo la historia wana hatari ya kuirudia.”
Somo hili linawaelezea Israeli wa kale—lakini
pia linaelezea ulimwengu mpya wa leo. Kwa sababu Isareli hawakudumu katika
njia, hatimaye walitekwa mateka, wakapotea kutoka katika historia! Baada ya
kutekwa nyara na kuadhibiwa mara moja zaidi, unabii unafunua kwamba Kristo
atawakusanya kwa mara ya mwisho wakati wa Kurudi Kwake.
Mfano Mmoja wa Mwisho
Biblia husema kuwa Mfalme Sulemani alikuwa
ndiye mtu mwenye hekima sana aliyewahi kuishi. Bado, alifanya kosa ambalo Mungu
aliliona ni kubwa sana kiasi kwamba, baada ya kifo chake, Alimwadhibu Sulemani
kwa kuuondoa ufalme kutoka kwa mtoto wake.
Kosa lake?
Alioa mwanamke aliyemwongoza katika kumwabudu
Isita (Ashtorethi). Angalia 1 Wafalme 11:4-6: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa
mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine...Kwa kuwa Sulemani
akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni…Sulemani akafanya yaliyo mabaya
machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.”
Mafungu ya 11-12 yanaonyesha kwamba ufalme ulichukuliwa kutoka kwa mtoto
wake.
Makanisa Mawili: Badiliko Kubwa
Yako makanisa mawili tofauti kabisa katika
Agano Jipya. Moja, ambalo ni Kanisa la kweli alilolijenga Yesu, linaelezewa
kama mke wa Kristo, likiacha kujihusisha na ulimwengu huu katika desturi zake
ili liwe safi bila waa lolote Anapokuja kwa ajili yake. Lakini, katika Agano
Jipya lote, ilihubiriwa kuwa waalimu wa uongo watajiingiza na kushika uongozi
wa ushirika wa kanisa. Wakristo wa kweli walilazimika kuzikimbia shirika zao
nyingi za awali ili waendelee kumtii Mungu. Kwa namna hiyo basi, walikuwa
“kundi dogo,” wakati wote wakiwa wametawanyika, kamwe hawakuwa na nguvu za
kisiasa katika ulimwengu huu.
Ulimwengu umefuatilia kidogo sana nyendo za
Kanisa hili dogo, lililotawanyika, lililoteswa,
lakini Kristo aliahidi kwamba hataliacha au
kulisahau na kwamba “milango ya kuzimu [kaburi] haitalishinda” (Mat. 16:18).
Japokuwa kwa vipindi lililazimika
kutawanyika kwa ajili ya maisha yake (Matendo 8:1; Dan. 12:7), Kristo ametunza
ahadi yake ya kubaki nalo kwa uaminifu, akiliwezesha na kulitia nguvu kwa njia
ya Roho Mtakatifu.
Pamoja na mateso ya kudumu—hata vipindi vya
mauaji makuu yaliyofanywa na makanisa makubwa maarufu ambayo wakati wote
yametafuta kuliangamiza—kundi dogo limeendelea kusalia wakati wote kwa miaka
karibu 2,000 iliyopita. Limeendelea “kushika amri za Mungu, na imani ya Yesu” (Ufu. 14:12).
Wakati wote Mungu ameliamuru Kanisa Lake
kutotunza sikukuu za kipagani! Kanisa hili dogo limehiari kumtii Mungu wakati
wote. Sura nzima iliyopachikwa ya Ufunuo 12 hutoa angalizo fupi la historia
yake, mpaka kipindi ambacho Mungu hulilinda muda mfupi kabla ya Kurudi kwa
Kristo.
Paulo aliuonya ushirika wa Wathesalonike, “…ile
siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi” (2 Thes. 2:7). Siri hii tayari
ilishaanza kuwa na ushawishi ndani ya Kanisa la kweli miaka ishirini tu baada
ya Kristo kulisimamisha katika mwaka 31 B.K. Ilikuwa ni hiyo hiyo siri ya
Wakaldayo, iliyofungamanishwa katika Krismasi na Isita—sikukuu zake kubwa
mbili! Mara kwa mara, kuwasili kwa sherehe hizi kuliwalazimu Wakristo wa kweli
kukimbia.
Ni katika mkondo huu huu unaotenda kazi ndio
umesababisha kijitabu hiki kiandikwe. Tangu kufariki kwa Herbert W. Armstrong
(kiongozi wa Kanisa la Mungu kutoka mwaka 1934 hadi 1986), “ule ukengeufu” uliotabiriwa
(neno la Kigiriki apostasia
hapa humaanisha “kuiasi kweli”) kutokea kabla ya Kurudi kwa Kristo (2
Thes. 2:1-3) sasa ulishatokea. Maandishi mengi ya bwana Armstrong hayapo tena
na yote yameandikwa upya na Kanisa la Mungu Rejeshwa.
Hivyo, shirika la Kanisa la kweli
lililoelezewa hapo kabla liliungana na lile kanisa lingine,
lililoonyeshwa kama malkia kahaba (kama Semiramisi/Isita) akimpanda mnyama
mwenye vichwa saba (Ufu. 17). Vichwa hivi huwakilisha historia ya kuibuka kwa
Himaya Takatifu ya Kirumi. Mwanamke huyu kahaba ni alama ya kanisa lenye nguvu
lililojijenga kisiasa. Taratibu, kanisa hili, likiwa na makao yake makuu
Roma, lilichukua na kutendea kazi mafundisho ya kipagani zaidi na zaidi hadi
kufikia wakati ambapo tofauti yake na dini ya kipagani ikawa ni matumizi yake
ya jina la Yesu Kristo. Hivi ndivyo Isita ilivyoanza kusherehekewa mahali pa
Pasaka ya kweli ya Kikristo.
Hili “kanisa mama” lina “mabinti madhehebu”
wengi, na mfumo mzima hujificha chini ya bendera ya “Ukristo”, wakati kwa
hakika ni “Dini ya Kisiri ya Kibabeli.” Biblia humwonyesha kama mdanganyifu wa
watu wote pamoja na nchi zote za Kikristo zikiwa zimeleweshwa na mafundisho
yake ya uongo! Anaonyeshwa kama aliyelewa kwa damu ya watakatifu, wakati huo
huo, akijidai kwamba yeye ndiye kanisa la kweli. Mambinti zake wote wamerithi
matendo yake ya kipagani.
No comments:
Post a Comment