KUINUKA na KUANGUKA
kwa HIMAYA
Katika kumbukumbu za
historia ya mwanadamu, kupangilia matukio na kuinuka na kuanguka kwa himaya, ni
kitu kinachoonekana kuwa kinaamuriwa na utashi, nguvu, tamaa, na uwezo wa
mwanadamu. Lakini katika neno la Mungu, pazia linaondolewa, na tunatazama
kupitia mchezo wa kuinuka na kuanguka wa matukio ya mwanadamu, wakala Mmoja
alieye na rehema, kwa uvumilivu akifanya kazi kutimiza mashauri ya mapenzi
yake.
Hakuna sehemu yoyote katika Maandiko
kulipo na kanuni hii ikiwa imefunuliwa wazi zaidi kuliko katika sura ya pili ya
Danieli. Hapa inaletwa machoni kwetu picha yote ya historia kuanzia wakati wa
Danieli mpaka siku zetu za leo.
Katika kipindi ambacho matukio haya
yalikuwa yanatukia, mfalme Nebukadneza na ufalme wake wa Babeli ulitawala
ulimwengu mzima wa wakati huo.
Usiku mmoja mfalme alikuwa anashangaa juu
ya kile ambacho kingefuata baadaye. Wakati akiangalia kwenye mji huu mkuu
aliotawala juu yake, inaonekana kana kwamba ulikuwa hauonekani; na wakati huo
hazikuwepo silaha [mashine] za vita za kuweza kubomoa kuta zake. Kuzunguka
ukuta kulikuwa na shimo kubwa dhidi ya wavamizi lililofanywa na Mto Frati. Mto
ulipita katikati ya mji, lakini kwenye sehemu ulipoingilia mjini, kulikuwa na
malango makubwa yakienea hadi majini. Nyuma ya hayo malango zilikuwepo kuta
zikizuia maji, kukiwa na malango ambayo yaliwezesha mtu kuingia mjini kwa njia
ya mto. Malango haya yangefungwa imara kwa milango mikubwa ya shaba, kwa hiyo
hata kama mtu angeweza kupita ng’ambo ya malango kwenye kuta hakukuwepo
uwezekano wa kuingia mjini mpaka malango ya shaba yafunguliwe.
NDOTO YA MAANA SANA
Wakati akitafakari mambo haya na
akishangaa kama ufalme wake ungedumu milele, Nebukadneza alilala usingizi.
Usiku ule alikuwa na ndoto ya maana, lakini alipoamka alikuwa hawezi kukumbuka
kitu chochote. Alihisi hata hivyo, kuwa hii ndoto kwa namna fulani ilikuwa na
majibu kwa swali lake juu ya mambo ya baadaye.
Mara moja Nebukadneza aliwaita wenye
hekima katika utawala wake kumsaidia akumbuke ndoto yake--haijalishi ni kiasi
gani cha umizimu wao, unajimu, uchawi, au ulozi walihitaji kutumia. Wenye
hekima walikusanywa, lakini hawakuweza, kupitia elimu ya mambo yote haya,
kufunua ndoto ya mfalme. Akiwatambua hawa wenye hekima kuwa walikuwa
wadanganyifu na kuwa wasingemsaidia, mfalme alikasirika na kuamuru wakamatwe na
kuwekwa kizuizini wakisubiri kuuawa. Danieli na wenzake walidhaniwa kuwa wenye
hekima, lakini hawakuitwa au kuwepo mbele ya mfalme. Hata hivyo, bado
walijumuishwa katika kukamatwa wenye hekima kwa kijumla.
Danieli alikata rufaa ili hatua hii ya
kuuawa icheleweshwe, akiahidi kuwa baada ya muda mfupi angempatia mfalme habari
alizokuwa anazitaka. Usiku ule yeye pamoja na wenzake waliweka ombi lao kwa
bidii mbele za Mungu ili kujua ndoto ya mfalme na tafsiri yake. Walijua kwamba
Mungu huwaheshimu wale wanaoweka tumaini lao lote kwake, na kwa hiyo walienda
kulala wakiamini kwamba Mungu angefanya mapenzi yake yatimie. Usiku ule Mungu
kwa rehema alifunua ndoto ya mfalme kwa Danieli, na hali kadhalika
ilichomaanisha, hivyo ikionyesha kwamba Mungu pekee anajua ya mbeleni.
SURA YA SANAMU YA FALME
Ndoto hii ya maana ilikuwa juu ya sanamu
kubwa ambayo kichwa chake kilikuwa cha dhahabu. Kifua chake na mikono vilikuwa
vya shaba. Miguu yake ilikuwa chuma, na nyayo zake na vidole vyake [pia]
vilikuwa mchanganyiko wa chuma na udongo (angalia Danieli 2:28-33). Kichwa cha
dhahabu kilitafsiriwa wazi wazi kuwakilisha Babeli (angalia Danieli 2:37-38).
Chini ya Nebukadneza, Babeli ilikuwa imekusanya dhahabu kutoka katika mataifa
yote iliyoyateka, [dhahabu hii] ikiifanya kuwa taifa tajiri sana la zamani.
Lakini hiyo haiko katika ukuu wa utajiri
unaodhaniwa, au katika hali ya kutoonekana ambayo mataifa au watu wanaweza
kupata nguvu, bali katika kujua na kutimiza mapenzi ya Mungu. Na hatima yao
inaamuriwa na mtizamo wao kwa makusudi ya Mungu kwao.
Ufalme wa Nebukadneza uliishia tu wakati
wa utawala wa mjukuu wake Belshaza, wakati taifa la pili, lililowakilishwa kwa
kifua na mikono ya shaba, lilipongia katika uwanja wa kutawala. Kwa ujumla, ni
ufalme ulio hodari zaidi ambao unashinda ule ulio dhaifu, lakini unabii
unaonyesha kwamba hii isingekuwa utaratibu wa mambo (angalia Danieli 2:39).
Katika sanamu, historia ya mataifa iliendelea kuanzia kwenye kichwa hadi kwenye
miguu, na kila badiliko liliakisiwa kwa madini dhaifu yakilinganishwa na yale
ya taifa lililotangulia.
BABELI YAANGUKA
Majeshi shirikisho ya Waamedi na Waajemi
yaliushambulia na kuushinda ufalme wa Babeli, kumwua Belshaza--mfalme wa mwisho
wa Babeli, na kisha Dario Mmedi alitawala katika sehemu yake (Angalia Danieli 5:28-31).
Zaidi ya karne moja kabla, Bwana alikuwa
amefunua kupitia Isaya mbinu ambayo kwayo Babeli ingechukuliwa na mtu ambaye
kupitia uongozi wake jambo hili lingetokea (angalia Isaya 44:27-28; 45:1-2).
Chini ya uongozi wa Koreshi Mwajemi, majeshi ya Waamedi na Waajemi, yaliweza
kubadilisha mkondo wa maji ya Mto Frati kwa muda kidogo. Wakati wa kipindi hiki
waliingia mjini kwa kutumia njia ya maji ambayo waliyakausha. Hata juhudi zao
zisingekuwa na maana, kama malango ya shaba yasingekuwa yameachwa wazi, bila
kulindwa na walinzi wanaotetea [ufalme], wakati mfalme na wakuu wake
walisherekea na kunywa (angalia Danieli 5).
Kama tu fedha ilivyo dhaifu kwa dhahabu
kithamani, basi Waamedi--Waajemi walikuwa dhaifu kwa utajiri na anasa. Wakati
Himaya ya Waamedi--Waajemi ilikuwa na nguvu katika mambo ya vita na eneo
walilokalia, haikuweza kuizidi Babeli katika kujilimbikizia utajiri au elimu.
Himaya ya Waamedi/Waajemi ilikuwepo kwa karibu miaka mia mbili, kuanzia 539 KK
hadi 331 KK.
Ufalme uliofuata, ule wa shaba,
ungewakilisha hatimaye ufalme ulioiangusha Uajemi. Tunajua kutokana na historia
kwamba ilikuwa ni Wayunani, chini ya Alexander Mkuu, ambaye katika mapigano
matatu ya nguvu (Granicus, mwaka 334 KK; Issus, mwaka 333 KK; na Arbela, mwaka
331 KK) aliyashinda majeshi ya Waajemi, akiifanya Uyunani Himaya ya baadaye.
Ukweli huu wa kihistoria unaonyeshwa pia waziwazi katika njozi nyingine na
Danieli, ulioko kwenye kumbukumbu katika sura ya 8, ambapo inaelezwa ufalme wa
kuwashinda Waajemi ungekuwa Uyunani (angalia Danieli 8:2-8, 20-21). Shaba
yalikuwa ni madini yaliyotumiwa na Wayunani kote, na pia yaliletwa katika
utengenezaji wa silaha na vyombo vya vita.
Roma, ambayo iliwakilishwa na miguu ya
chuma, iliyashinda majeshi ya Kiyunani katika vita vya Pydna mwaka 168 KK. Roma
hatimaye ilitawala ulimwengu kutoka mwaka 168 KK hadi 476 BK, wakati
ilipoanguka mwishoni kwa makabila ya kivamizi ya washenzi.
Kwa zaidi ya miaka 500, Roma ilionekana
kuwa isingeshindwa. Bendera zake zilipepea kutoka visiwa vya Uingereza mpaka
mto Frati, Kutoka Bahari ya Kaskazini mpaka Jangwa la Sahara. Makaisari wake
waliabudiwa kama miungu, na kwa uwezo wake ilifanya ulimwengu wote kama nyumba
moja ya kifungo. Katika maneno ya mwanahistoria Edward Gibbon, “Kupinga ilikuwa
ni hatari ya kifo, na isingewezekana kuruka.” The Decline and Fall of the Roman
Empire, gombo la 1, ukr. 190.
Wakati Roma ilipoanguka, eneo lake
liligawanywa katika sehemu kumi ambazo sasa zinafanya mataifa ya Ulaya. Kama
ambavyo chuma na udongo kwa sehemu vina nguvu na kwa sehemu dhaifu, kwa hiyo
ndivyo ingekuwa kwa mataifa haya kumi ya Ulaya ambayo nyayo na vidole vyake vya
sanamu hii ilichowakilisha. Kama ambavyo chuma na udongo haviwezi kuchanganyika
au kushikamana, kwa hiyo mataifa haya yenyewe yasingeungana kama dola ya
mamlaka inayotawala ulimwengu.
Kwa karne kumi na tatu za mwisho, watu
wenye nguvu wametafuta kuhuisha utukufu wa Himaya ya Kirumi ya zamani,
wakiunganisha pamoja mataifa mbalimbali ya Ulaya. Tukianza na Charlemagne na kuendelea
na Charles V, Louis XIV, Napoleon, Kaiser William II, na Adolph Hitler--wote
kwa ishara wameshindwa, japo kwa wakati lengo lilionekana kufikiwa. Maneno saba
madogo ya unabii yalisimama katika njia yao: “Hawatashikamana, kama vile chuma
kisivyoshikamana na udongo” Danieli 2:43. Na mataifa ya Ulaya, moja moja au
yote, hayatashikamana katika mamlaka ya kutawala ulimwengu tena!
NDOTO BADO HAIJATIMIZWA
Lakini hii haikuwa mwisho wa ndoto. Pia
ilifunuliwa kwamba katika siku za falme hizi, Mungu wa mbinguni atasimamisha
Ufalme wake wa milele. Ufalme huu wa haki, uliowakilishwa na jiwe [mwamba]
ambalo liligonga sanamu miguu yake, ungeendelea kukua mpaka dunia yote ijazwe,
na hakuna hata mamlaka moja ya dunia ambayo ingezuia (angalia Danieli 2:34-35,
44).
Ingawa wafalme wengi na mamlaka
zimejaribu kumharibu Kristo--aliyewakilishwa na Jiwe (angalia 1 Wakorintho
10:4), na wameendesha vita dhidi ya wafuasi wa ufalme wa Kristo wa haki, bado
hakuna hata [ufalme mmoja] uliofanikiwa na wala hakuna utakaofanikiwa. Kristo
na ufalme wake utatawala milele, utukufu wake na kweli utafunika na kuijaza
dunia hii kama tu maji yaijazavyo bahari (angalia Habakuki 2:14). Na mataifa
yote maovu ya dunia yatasagwasagwa kama unga wakati Kristo--Mwamba anapokuja
tena katika mawingu ya mbinguni.
BADO KUNA MUDA WA KUANGUKA KWENYE
JIWE
Rafiki, je utakuja kwa Kristo leo,
ukianguka juu ya Mwamba huu wenye nguvu na kuvunjika katika moyo, ukitubu
dhambi zako zote upate kuinuka na kuishi maisha mapya ukiwa na nafasi ya kuwa
na uzima wa milele ikiwa utakuwa mwaminifu hadi mwisho? Au utabaki na majivuno
na kutotubu, uking’ang’ania kwenye dhambi zako utakapokuwa umechelewa, na
kukutikana na Mwamba huu wa nguvu ukikuangukia na kukusaga mpaka kuwa
vumbi--bila nafasi ya uzima wa milele? Ndugu msomaji, je unataka kungukiwa na
Mwamba huu mkuu na kupotea? Au unataka kupata hifadhi na kujificha katika
Mwamba huu na kuokolewa? Uchaguzi ni wako.
“Ee Mungu, ukisikie kilio changu,
Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo,
Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda. Kwa maana ulikuwa kimbilio langu,
Ngome yenye nguvu adui asinipate.” Zaburi 61:1-3.
“Ingia ndani ya jabali; ukajifiche
mavumbini mbele za utisho wa BWANA, mbele ya utukufu wa enzi yake.” Isaya 2:10.
“Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike
milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe
kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda siku zote. Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.” Zaburi 71:1-3.
“Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala
yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.” Yohana 6:37.
Ili kupata habari zaidi juu ya mada hii muhimu, tafadhali bonyeza
hapa
No comments:
Post a Comment