MABADILIKO YA SIKU ZA IBADA SURA YA 2

SURA YA 2
SABATO NA BIBLIA

Mwasisi wa Sabato ndiye Mwasisi wa dini ya Kikristo - Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.
Yeye ndiye aliyeiumba dunia hii, akiifanya kwa siku sita. Yeye ndiye aliyestarehe siku ile ya saba, na kuibarikia siku ile, na kuitakasa. Kwa maana Mwana wa Mungu alikuwa na hata sasa ndiye Muumbaji. Biblia inasema "Vyote vilifanyika kwa huyo."

" Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakukufanyika cho chote kilichofanyika" (Yoh 1:1-3).

 "Alikuwako ulimwenguni, hata kwa Yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua" (Yoh 1:10).  "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli" (Yoh 1:l4).

"Naye  ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa
kuwa katika  Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi,
vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka;
vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake" (Kol 1:15,16).

“Kama tulivyokwisha kuona tayari, wakati alipoifanya Sabato ulikuwa ni mwishoni mwa juma lile la uumbaji”. (Mwa 2:1-3).
Njia aliyoitumia kuifanya Sabato ilikuwa kwa kuchukua siku moja, siku ile  ya saba, na Yeye Mwenyewe kustarehe siku hiyo, kuibarikia, na kuitakasa.

SABATO NI SIKU, SIO KANUNI
Kifaa alichotumia kuifanya Sabato  ni siku ile ya saba.  Akaitwaa siku ile, na kuifanya Sabato. Sabato sio kitu fulani alichokiweka juu ya siku ile.  Ni siku ile  yenyewe. "SIKU ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako." Hatuamriwi kwamba tu"ikumbuke SABATO [ t]uitakase."  Amri inasema hivi: "Ikumbuke SIKU ya sabato uitakase." Sabato si kitu fulani kilicho tofauti na siku hiyo, ambacho kinaweza kusogezwa huku na huko na pengine kuwekwa juu ya siku nyingine. Ni siku yenyewe hasa, siku ile ya saba.

Siku hizi tunasikia mengi juu ya KANUNI ya Sabato. Lakini Biblia haizungumzi kamwe juu ya KANUNI ya Sabato. Hakuna kitu kama hicho cha KANUNI ya Sabato iliyobarikiwa na kutakaswa kwa faida ya binadamu, mbali na siku yenyewe. Ilikuwa ni SIKU yenyewe ambayo ilibarikiwa kwa kutakaswa; na kwa sababu hiyo ni SIKU hiyo ambayo inakuwa Sabato.

Siku ile aliyoibarikia Mungu kamwe haiwezi kutenganishwa  na Sabato.  Nayo Sabato haiwezi kamwe kuondolewa kutoka katika siku ile aliyoibarikia Mungu. Vitu hivi viwili haviwezi kutenganishwa. Havitengeki kwa sababu siku zote viko pamoja.

SIKU YA SABA ndiyo Sabato; Sabato ndiyo SIKU YA SABA. Yesu aliifanya Sabato kwa ajili ya taifa zima la kibinadamu, sio kwa ajili ya kundi moja tu ama taifa moja tu. "Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu" (Marko 2:27).

SABATO INADUMU MILELE
Mungu aliifanya Sabato kwa ajili ya wakati wote. Haikukusudiwa kuwa ya muda tu, bali ya milele. Kamwe hapatakuwa na wakati wo wote ambapo siku hii ya saba haitakuwa siku liyobarikiwa, siku ya Mungu ya kupumzika.  "Maagizo [amri] yake yote ni amini. Yamethibitika milele na milel.   (Zab. 111:7,8).

Hata katika nchi mpya Sabato ya siku ya saba iliyobarikiwa itaendelea kutunzwa na mataifa
ya wale waliookolewa. "Na itakuwa ... Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema BWANA" (Isa. 66:23).

Sababu kwa nini Mungu aliwaamuru wanadamu kuitunza siku ya Sabato ni hii: "Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya sabato akaitakasa" (Kut. 20:11).
Kwa hiyo, Sabato ni kumbukumbu ya uumbaji wa nchi hii kwa siku sita, naye Mungu ameiweka kama ishara ya uweza Wake wa Uumbaji. Kwa njia ya kuitunza Mungu alikusudia kwamba mwanadamu angemkumbuka Yeye daima kama Mungu wa kweli na wa pekee, Muumbaji wa vitu vyote.

SABATO INAONESHA ISHARA ZIFUATAZO KWA MWANADAMU
1.ISHARA YA UTAKASO
Uweza wa Mungu wa uumbaji ulitumika kwa mara ya pili katika kazi yake ya ukombozi, ambayo kwa kweli ni uumbaji mpya. Sabato kama kumbukumbu ya uweza wa uumbaji inakuwa kumbukumbu ya wokovu wetu katika Kristo. Iliwekwa dhahiri kama ishara ya utakaso. "Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye" (Eze. 20:12).

Kama Kristo  alivyo  Mmoja awatakasaye watu Wake, hivyo ndivyo Sabato inavyokuwa ishara ya vile Kristo alivyo kwa yule aaminiye.  Ni kumbukumbu ya pumziko letu kutoka dhambini, kumaliza kazi Yake ya wokovu kamili ndani yetu.  Kumbukumbu kama hiyo inadumu milele hata milele.

Ni Yesu anayeokoa kutoka dhambini. Wokovu huu kutoka dhambini ni utendaji halisi wa uweza wa Mungu wa uumbaji. Ni kwa njia ile tu ya uweza ulioletwa na Roho Mtakatifu kwa wenye dhambi, inaweza kushindwa dhambi katika mwili wa mwanadamu, na mwanadamu huyo kuweza kuingia katika pumziko hilo la imani. 
 Ni Yesu anayetoa pumziko hilo. "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, NAMI NITAWAPUMZISHA" (Mt. 11:28).

2. ISHARA YA UKOMBOZI KUTOKA DHAMBINI
Ishara ya uweza wa Kristo wa uumbaji ni Sabato. "Sabato maana yake pumziko.” Ilitolewa sio tu kwa ajili ya pumziko la  kimwili, bali kama ishara ya pumziko la kiroho na ukombozi kutoka dhambini. Kwa hiyo yule anayeitunza Sabato kwa akili ameingia katika raha yake Mungu, "Yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi Yake" (Ebr. 4:10).

Kwa njia hii Sabato, kwa yule aaminiye katika Kristo, inakuwa ishara ya yote yale ambayo Injili inayo kwa ajili yake katika Kristo.
3.NI MSINGI WA UKAMILIFU WA EDENI
Ni mojawapo ya mambo mawili yaliyosalia ya maisha yale ya Edeni ambayo yameendelea kuwako tangu Anguko lile,  jingine ni ndoa, na, kwa hiyo, ni mojawapo ya kanuni za awali za Edeni. Siku hii ya mapumziko hutokea kila juma, ili kuweka mbele yetu daima ukweli wa kustarehe kwake Mungu mwishoni mwa juma lile la  Uumbaji. Tunapaswa kumkumbuka Mungu kila siku, lakini Sabato inakuja kwetu kila juma, ikituletea nafasi nyingi za kupumzika, kutafakari, na kuzungumza na Muumbaji wetu. Kabla haijapoteza mibaraka yake na mambo yake ya thamani, kuja kwa Sabato nyingine huufanya mpya mvuto wake utakasao. Hivyo inazifanya siku zote kuwa za kupendeza na kuueneza mbaraka wake katika saa zetu zote, basi, na tu "IKUMBUKE siku ya sabato [t]uitakase."

MWANZO NA MWISHO WA SABATO
Sabato inaanza jua linapozama na kuisha jua linapozama [kesho yake].  Njia ya Biblia ya kuhesabu siku sio kuanzia usiku wa manane mpaka usiku wa manane [kesho yake], bali ni kutoka jioni hata jioni [kesho yake]. Jua linapozama siku inakwisha, na siku mpya inaanza.
Jioni ndio mwanzo wa siku.  "Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja" (Mwanzo 1:5). 

Yaani, jioni, au sehemu ya siku yenye giza, inakuja kwanza, nayo inafuatiwa na asubuhi, au sehemu ya siku yenye mwanga. Agizo la Mungu ni kwamba, "tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo sabato yenu" (Law. 23:32) "Jioni" inaanza jua linapozama.  "Jioni, katika machweo ya jua"  (Kumb. 16:6). "Jioni, na jua limekwisha kuchwa" (Mk. 1:32).

Kwa hiyo, jua linapozama jioni siku ile ya sita ya juma, huo ndio mwanzo wa Sabato ya Mungu. Ijumaa jioni jua linapozama huo ndio mstari unaogawa wakati mtakatifu."BWANA AKAIBARIKIA siku ya Sabato AKAITAKASA"   (Kutoka 20:11).

Ni wakati huo mtakatifu tunaoagizwa kwamba tuu"kumbuke" ili  ku"[u]takas[a]." Mungu
aliifanya TAKATIFU; anamwamuru mwanadamu KUITAKASA. KUSUDI LA KUITUNZA SABATO. Kuitakasa Sabato ni kuitumia kwa kusudi lile lile   liyowekewa.  Ilikusudiwa kuwa siku ya ibada kwa wote pamoja na maombi ya faragha.  "Siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa, KUSANYIKO TAKATIFU"  (Law 23:3).
Tunacho kielelezo cha Yesu Mwenyewe akihudhuria ibada siku ya Sabato: "Na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi Yake" (Lk 4:16). Maandalio ya kuitunza vizuri Sabato ni pamoja na kupika chakula na kuandaa vitu vingine vinavyoweza kuhitajika ili kuwa tayari kuacha kufanya kazi za kawaida, za kidunia wakati Sabato inapoanza, na kuutumia muda wetu kwa mambo matakatifu, ya  mbinguni
 (Kut.16:22,23; Lk. 23:54).
Sabato sio siku ya kufanya kazi za kawaida, wala uzembe, wala burudani. Ni kwa ajili ya kupumzika, kiroho na kimwili; kwa ajili ya kutafakari; ibada ya faragha na ya wote; kwa ajili ya furaha takatifu, na kwa kusaidiana. Ilikusudiwa kuwa siku ya furaha, uchangamfu, na bora kuliko zote katika zile siku saba.

SABATO YA AGANO JIPYA
Agano Jipya halibadilishi hata kwa kiwango kidogo mno wajibu wetu wa kuitunza siku ya saba iliyoamriwa na Mungu. Kristo aliitunza siku hii katika kipindi chote cha maisha Yake hapa duniani. Wanafunzi wake waliitunza barabara siku hii katika kipindi chote cha maisha yao, wakati wanaanzisha makanisa ya Kikristo ya mwanzo. Hakuna tukio hata moja katika kumbukumbu za Agano Jipya ambapo binadamu awaye yote alijaribu kuitunza siku ya kwanza kama Sabato.
Sabato ya Agano Jipya ni Sabato ile ile ya Agano la Kale, yaani, siku ya saba ya juma. Ambapo pia Yesu mwenyewe aliikua akiiadhimisha siku hiyo “Na siku ya Sabato [Yesu] akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi  yake.” (Luka 4:16 )
 Ulimwengu wote wa Kiyahudi katika siku zile za Yesu uliitak asa Sabato ya  Mungu ya siku ya saba. Kwa kweli, Wayahudi wameendelea daima kuitunza Sabato ya siku ya saba.

Ahsante, Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment