UKIIFAHAMU KWELI ITAKUWEKA HURU

UKIIFAHAMU KWELI ITAKUWEKA HURU
Amani iwe nawe mwana wa Mungu.
Natumai neema ya Mungu imekufunika kipekee kwa juma zima lililoisha. Ni jambo jema kumshukuru Mungu kutupigania kwa wiki nzima. Maombi yangu yako nawe mpendwa wangu kwamba Bwana akufanikishe ktk kila jambo jema utakalolitia mikononi mwako kwa wiki hii. Damu ya Yesu inenayo mema ikanene mema katika maisha yako kwa namna ya tofauti wiki hii. Natumai kama ambavyo umepanga ratiba za majukumu mbalimbali naamini utakuwa umejipangia ratiba ya kukaa magotini na Baba kumpangia dua na sala zako kwa juma hili.
Ndugu yangu maandiko yanasema kwamba:
‘Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo. Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu’ Yohana‬ 8:31-47
Mpendwa wangu hakuna jambo zuri katika maisha kama mtu kuwa huru. Kuwa huru kifikra, kiroho, na kimwili. Mwanadamu siku zote anatafuta uhuru wa kufanya mambo fulani fulani maishani mwake. Anataka awe na uhuru wa kujieleza n.k
Bwana anatuambia tukilijua neno lake hakika tutakuwa huru. Ni hakika na kweli. Ndugu zangu ikifika mahala tukalijua neno la Mungu itatusaidia kutufungulia milango ya minyororo tuliyofungwa kwenye fikra zetu. Kwa mfano katika madhehebu yetu tunafundishwa baadhi ya mambo ambayo yanatufunga sana. Wakati mwingine hayatupi uhuru wa kuifanya kazi ya Mungu kwa uhuru unaotakiwa. Wakati mwingine unatufanya tusiweze hata kushirikiana na watu wengine kabisa.

Mchungaji mmoja wa kanisa fulani alikuwa na huduma nzuri sana na maombi na maombezi kwenye local church yake. Si utaratibu wa kanisa lao kuwa na huduma ya maombezi. Kwa hyo akaanza kupangiwa mipango kuwa yuko kinyume na utaratibu wa kanisa. Askofu wake alivyokuja kuona huduma ile alifanyiwa mizengwe ya kufukuzwa kazi. Katika kujitetea akamwambia Askofu kosa langu liko wapi? Maana nimegundua katika maandiko watu wakiombewa kwa jina la Yesu wanapokea uponyaji, sasa kwanini kunizuia?
Nilishawahi kuona mahala pengine watu wamejitambua kwamba kunena kwa lugha ni moja ya karama ya Roho Mtakatifu. Watu fulani wakajibidiisha kuomba na wakapewa kipawa hicho. Lakini ilileta shida kwenye kanisa maana kanisa lile walikuwa hawaamini katika kunena kwa lugha. Wakaanza kuonwa kana kwamba wameleta elimu isiyokubalika ndani ya kanisa na kuanza kuitwa majina ya ajabu ajabu.
Waangalie waisraeli katika neno hilo hapo juu jinsi walivyokuwa wamefungwa katika fikra zao kiasi kwamba walipata shida mno kuelewana na Bwana Yesu kwa wakati wake wote wa huduma. Kila ambacho Bwana Yesu alikuwa akikifanya kilionekana kigeni na machukizo kwa hawa watu kwa sababu tayari walikuwa wamekariri mambo fulani fulani vichwani mwao hata walipofafanuliwa hawakuwa tayari kuelewa.
Ndugu zangu tusipojitambua kwa kulifahamu neno la Mungu tutaishi katika vifungo vingi sana. Vifungo vya kifkra ni vibaya zaidi. Maana shetani hupitia humo kawatesa watu hadi kimwili. Maana ufahamu wa mtu unapokuwa umefungwa adui aweza kufanya lolote katika mwili na mtu asijitambue.
Nilipata kukutana na watu mahala fulani walikuwa wamefungwa na mafundisho fulani. Walikuwa wamefundishwa kwamba hawapaswi kushirikiana na mtu yeyote asiye wa kanisa lao! Yani hawaruhusiwi hata kuongea nao!
Ni wito wangu kwako ukae chini na kuwa na utaratibu mzuri wa kujifunza neno la Mungu kila siku ili likuweke huru, tena taratibu wala usiwe na haraka. Jifunze taratibu na utaona namna gani Roho wa Mungu atakusaidia kujifunza wakati mwingine hata vitu ambavyo umeishi kanisani miaka nenda rudi hukuwahi kujifunza. Kaa na Roho Mtakatifu akufundishe neno. Maana ukilijua neno litakuweka huru. Halitakufunga hata unapokutana na mtu mwingine.

No comments:

Post a Comment